Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila
mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapema
sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo
imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa
fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi
wangu.
Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka
mitano na nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi
kama kilele kimojawapo cha maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila
siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele
mipaka ya ujuzi na elimu. Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika
lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo
wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali
zinazoikabili dunia yetu.
No comments:
Post a Comment