Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Napenda
kuwatangazia wana-Bumbuli kwamba ile ahadi niliyotoa wakati wa kampeni
– ahadi ya kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli – imetimia. Shirika
limepata usajili, limefungua ofisi, lina watumishi wa mwanzo na tayari
ipo miradi minne ambayo utekelezaji wake utaanza mara moja. Tutazindua
Shirika hili tarehe 4 Agosti 2012, katika mkutano wangu na
wana-Bumbuli waishio Dar es Salaam na mikoa ya jirani, na baadaye
katika mikutano na wananchi jimboni Bumbuli.
Chimbuko
Nilipoamua
kugombea Ubunge wa Bumbuli mwaka 2010, niliamua kwamba katika utumishi
wangu kama Mbunge nitashirikiana na Wana-Bumbuli pamoja na marafiki na
washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi katika kuleta mageuzi
ya kiuchumi na kijamii Bumbuli. Jimbo letu ni kati ya majimbo yaliyo
nyuma kimaendeleo kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhitaji jitihada za ziada
– zaidi ya zile za Serikali. Katika kufikia lengo hilo, niliahidi
kuanzisha Shirika litakaloratibu shughuli za maendeleo katika Jimbo.
Nilifikia
uamuzi wa kuanzisha Shirika nikitambua kwa dhati uwepo wa jitihada
nzuri za serikali katika kuboresha maisha ya watu wa Bumbuli nikitegemea
pia serikali kuendeleza jitihada zaidi. Hata hivyo natambua kwamba
kazi ya maendeleo si kazi ya serikali pekee, inahitaji ushiriki wa kila
mmoja na hasa sekta binafsi ili kuisadia juhudi za serikali kufikia
malengo ya maendeleo. Nilitaka kuchambua uwezo wa watu binafsi,
wafanyabiashara na taasisi mbalimbali katika kupanua wigo wa ajira na
shughuli za kipato kwa watu wa Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii.
Mpango wa Mageuzi Bumbuli
Mpango
huu ulitokana na mawazo niliyokuwa nayo nilipoamua kugombea ubunge juu
ya haja kuunganisha jitihada za wenyeji wa Bumbuli, wafanyabiashara na
taasisi za hapa nchini, na wawekezaji kutoka nje katika kufanikisha
mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Niliamini jitihada za sekta binafsi
zikioana na mipango ya maendeleo ya serikali kutachochea kasi ya ukuaji
wa uchumi wa wana-Bumbuli na hivyo kupanua wigo wa ajira na shughuli za
kibiashara za uzalishaji mali katika Jimbo.
Malengo ya mpango wa kuikwamua Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii ni kama ifuatavyo:
1. Kuongeza
pato la wakulima wa Bumbuli kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha
mbinu za kilimo, mbinu za kuhifadhi mazao, na hatua mahsusi za
kuongeza thamani ya mazao hayo (value-addition).
2. Kuwavutia
wawekezaji kujenga taasisi au shule itakayokuwa na wanafunzi, walimu
na wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa Bumbuli,
hivyo kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
3. Kuleta
huduma za kifedha kwa kuanzisha taasisi ya fedha Bumbuli ambayo
hatimaye itakuwa benki ya wananchi wa Bumbuli ambayo itatoa mikopo kwa
masharti nafuu.
4. Kuchukua
hatua mahsusi za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani
maisha na maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Bumbuli yanategemea sana
mazingira na mandhari ya milima ya Usambara.
5. Kuanzisha
Shirika la Maendeleo Bumbuli litakalokuwa na jukumu la kubuni,
kuratibu na kusimamia uendeshaji wa shughuli zilizoainishwa hapo juu.
Shirika hili ndilo litakalokuwa kiini cha mtandao wa kijamii wa uchumi
kwa Bumbuli.
Malengo
haya yamekusudiwa kuwanufaisha wananchi kwa kuanzisha mtandao wa
kimataifa wa kibiashara ambapo wadau mbalimbali watashiriki; na hatamu
za uchumi zikishikiliwa na watu wa Bumbuli wenyewe.
Shirika la Maendeleo Bumbuli
Shirika
la Maendeleo ya Bumbuli ni shirika la maendeleo lisilotengeneza faida
lenye lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Jimbo. Shirika
hili limesajiliwa kama kampuni yenye ukomo wa dhamana, na litafanya
biashara ili kulipia gharama za uendeshaji na faida inayopatikana
itatumika kugharamia miradi ya maendeleo ili kufikia malengo ya kijamii
ya Mkakati wa Mageuzi ya Uchumi wa Bumbuli. Shirika litakuwa na kazi
zifuatazo;
1. Kuihamasisha
sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya Bumbuli kwa kuwekeza
katika maeneo mblimbali. Uwekezaji huu utahusisha wafanyabiashara wa
ndani na wale wa kigeni na Shirika litajihusisha zaidi katika kutoa
msaada wa kitaalamu, na kuratibu mtandao wa kibiashara utakaoenea
kuanzia ngazi ya wilaya, taifa na kimataifa.
2. Kubuni
na kuitangaza ‘Chapa Lushoto’ (Lushoto Brand) pamoja na kutayarisha
mafunzo kwa wakulima juu ya kutayarisha mazao yao ili yapate kuwa na
thamani bora zaidi. Shirika hili litajenga mfumo utakaosaidia kununuliwa
kwa mazao ya wakulima na masoko ya bidhaa, muundo utakaotumiwa na
wafanyabiashara binafsi.
3. Kuvutia
uwekezaji kwa njia ya kuitangaza Bumbuli pamoja na kuishauri
halimashauri na serikali za mitaa kuhusu maeneo ya kuwekeza na
miundombinu ya kuboresha ili kuvutia uwekezaji zaidi.
4. Kutafuta
fedha kwa ajili ya uwekezaji wa kijamii na kibiashara na kutoa msaada
wa kihuduma kwa makampuni ya biashara ya nyumbani na uwekezaji wa
kutoka nje.
5. Kuratibu mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wadau mbalimbali wa maendeleo Bumbuli.
6. Kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mpango wa Maendeleo na Mpango wa uwekezaji.
Shirika
litaongozwa na bodi itakayokuwa na watu kati ya nane na kumi na moja
na kuendeshwa na timu ya watu watano ambao watakuwa ni, Mkurugegenzi
Mtendaji, Mweka Hazina, Wachambuzi wawili na Mhasibu.
Miradi ya Mwanzo ya Shirika la Maendeleo Bumbuli
1. Mradi
wa Kituo cha Kukusanya, Kusafisha, Kugredi, Kupaki na Kutafuta Masoko
ya Mboga na Matunda ya Bumbuli (Bumbuli Packing House)
Wilaya
ya Lushoto, jimbo la Bumbuli likiwemo, inasifika kwa kilimo cha mboga
na matunda. Hata hivyo, asilimia hamsini (50%) ya mboga na matunda
yanayolimwa Bumbuli yanaharibika – kwa kutokufika sokoni au kutopata
soko la uhakika. Hata yale mazao yanayonunuliwa, wakulima wanapata
mapato kidogo sana ambayo hayaendani na thamani ya jasho lao.
Mradi
wa Bumbuli Packing House, ambao utajiendesha kibiashara, una dhamira
ya kumaliza tatizo hili. Pamoja na hili mradi huu utawawezesha wakulima
kwa pembejeo – mbegu, mbolea, pampu, nk – na mafunzo ili wazalishe
mboga na matunda bora zaidi ya kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.
Mradi
huu, katika awamu ya kwanza, utagharimu shilingi milioni 780. Utafiti
wa Kibiashara (Market Analysis Survey) umefanyika, Andiko la Kibiashara
limekamilika. Na majadiliano na wadhamini kupata fedha hizi yamefikia
mwisho ambapo ndani ya mwezi mmoja fedha hizo zitapatikana, na baada ya
maandalizi kukamilika (ikiwemo kupata professional management), mradi
utaanza.
2. Mradi wa Kiwanda cha Kusindika Mboga na Matunda
Shirika
liko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kukifufua upya kiwanda
cha kusindika Mboga na Matunda (Natural Choice) kilichopo Soni, jimbo
la Bumbuli, ambacho mwanzoni kwa miaka ya 2000 kilikuwa na sifa kubwa
ya kutoa bidhaa nyingi, bora na za thamani kubwa.
Mradi
huu utaenda hatua ya mbele zaidi ya Bumbuli Packing House kwa
kutengeneza juisi, jams, concentrates na bidhaa nyingine za mboga na
matunda kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi. Mradi huu, sio tu
utatoa ajira kwa watu wa Bumbuli, bali pia utahakikisha soko la uhakika
kwa mboga na matunda ya Lushoto linapatikana na kuongeza thamani ya
mazao ya wakulima na hivyo kuwaongezea kipato.
3. Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Masharti Nafuu (Bumbuli Microfinance Institutition)
Jimbo
la Bumbuli halina tawi la benki yoyote na huduma ya fedha ni tatizo
kubwa. Shirika la Maendeleo Bumbuli limeomba leseni kutoka Benki Kuu
kuanzisha taasisi ya fedha kwa ajili ya ukopeshaji kwa masharti nafuu na
pamoja na huduma nyingine za fedha. Andiko la Mradi huu limefanywa
kitaalam sana, baada ya utafiti wa karibu miezi nane kuhusu njia muafaka
ya kutoa huduma ya fedha kwa masharti nafuu kwa watu wa Bumbuli. Mradi
huu utagharimu shilingi milioni 450 kwa kuanzia na baada ya miaka
mitatu mtaji utaongezwa na kufikia shilingi bilioni 1.6. Wakati
tunasubiri usajili na leseni kutoka Benki Kuu tayari wapo wafadhili
ambao, baada ya kusoma andiko letu, wameonyesha nia ya kusaidia mradi
huu.
Msingi
wa mradi huu ni kuwezesha vikundi vya kuweka na kukopeshana fedha
ambavyo tayari vipo lakini vina mtaji mdogo, kutoa mafunzo ya fedha kwa
vikundi hivi, na kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vingine. Kipaumbele
na nafuu ya mikopo itatolewa zaidi kwa vikundi vitakavyotumia fedha
hizi kwa uzalishaji mali na shughuli ambazo zitaajiri watu wengine.
4. Mpango wa Malipo kwa Kufanya Vizuri kwa Shule za Sekondari (Cash-On-Delivery for Secondary Education in Bumbuli)
Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) litakavyotekeleza program ya msaada ya Malipo kwa kufanya vizuri** au cash on delivery
(COD), ambayo itaongeza umakini na tija kwenye kujifunza na matokeo ya
mitihani katika shule za sekondari jimboni Bumbuli. Kulingana na
utafiti wetu, jimbo la Bumbuli liko kwenye hali ya kukata tamaa ya
kupata msaada kwenye Sekta yake ya Elimu ya Sekondari. Shirika la
Maendeleo Bumbuli (BDC) litatekeleza program ya majaribio ya malipo
kwa kufanya vizuri (COD), ya miaka mitatu ambayo itafanya malipo
kulingana na idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu Mitihani ya Taifa ya
Kidato cha Nne. Shirika la Maendeleo Bumbuli (BDC) linalenga kuboresha
matokeo ya kujifunza/elimu katika jimbo la Bumbuli kupitia program hii
ya kutoa motisha. Program hii itahusu Shule za Sekondari za Serikali za
Kata.
Malipo
kwa kufanya vizuri (COD) ni utaratibu mpya kutoa msaada ambapo
wafadhili hutoa pesa kwenye maendeleo yanayopimika kwa kuangalia
matokeo maalum. Unahusianisha moja kwa moja malipo na matokeo maalum,
ikiwapatia watendaji/wapokeaji motisha ya kuongeza nguvu zao za
kufanyakazi ili kufikia maendeleo.
Msingi
na uhalali wa wazo la CDO, ulioanzishwa awali na Kituo cha Maendeleo
ya Kimataifa(Center for Global Development) mjini Washington, umejikita
kwenye mtazamo kwamba kazi za maendeleo ni lazima zitathminiwe kwenye
athari (impact) zinazoletwa. Mbinu inawakilisha mabadiliko kutoka
kufuatilia nguvu na rasilimali ambavyo mashirika huwekeza katika kutoa
misaada - 'nyenzo/rasilimali', na pia shughuli na vifaa/vitendeakazi
vinavyotokana na uwekezaji huo - 'matokeo'. Badala yake, mbinu hii
inalenga kujikita kuangalia namna gani maisha ya watu masikini yameweza
kubadilishwa kutokana na uwekezaji kwenye sekta au eneo fulani la
maendeleo (afya, elimu, n.k).
Mnamo
mwezi Septemba 2011, Shirika la Maendeleo Bumbuli lilifanya utafiti wa
kina juu ya mazingira ya kujifunzia Bumbuli na kugundua kwamba shule
nyingi, walimu, na wanafunzi wa Bumbuli hawana motisha wala rasilimali
zinazohitajika kuwawezesha wafanye vizuri kama inavyotarajiwa.
Kwa
wastani, kila shule iliyotoa data za matumizi ya pesa ilionyesha ni
Sh. 5,268 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka 2010 (kiasi kilichotarajiwa kwa
shule za Sekondari ni shilingi 25,000 kwa kila mwanafunzi). Pamoja na
hayo, utafiti ulionyesha kuwa ni 71% tu ya walimu walikuwepo shuleni,
ambapo ni 19% tu walikutwa madarasani. Utafiti huo ulionesha kuwa walimu
hupata mishahara yao kwa wakati. Wastani wa mshahara halisi wa mwalimu
wa Bumbuli ni Sh.395,000 kutoa malipo ya deni ya Sh.74,000 kila mwezi.
Wengi walionesha kuwa na shughuli ya ziada ya kiuchumi (67%), hasa
kilimo (90%). Wengi wao (98%) walidai kutokuhusishwa katika hatua za
kupanga bajeti za shule. Wastani wa Pato la Mtanzania anayeishi kijijini
(ikiwemo Bumbuli) ni Sh.152,000 (HBS, 2010). Wakati 89% ya wanafunzi
wanaonesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi wa familia, bado 70%
wanafanikiwa kupata muda kidogo wa kukamilisha kazi zao za masomo wakiwa
nyumbani, huku 34% inaonesha hawakufika shule kwa mwezi uliopita
kutokana na kusaidia shughuli za nyumbani. Matokeo ya Mtihani wa Kidato
cha Nne ya mwaka 2011 kwa Shule za Bumbuli yalikuwa mabaya sana. Kati
ya wanafunzi 1,327 waliofanya mtihani, hakuna aliyepata Division 1,
waliopata Division 2 ni wanne, waliopata Division 3 ni 39, na
waliobakia, yaani wanafunzi 1,274, walipata Division 4 na 0.
Pamoja
na hatua mahsusi ambazo Serikali inachukua kuboresha elimu nchini na
kuongeza ufaulu, Shirika la Maendeleo Bumbuli, kupitia Program hii ya
COD, linataka kuonesha kwamba fedha zinaweza kugawika vizuri na kwa
usahihi ili kuboresha elimu kwa kupima kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Hatua na mikakati inayopendekezwa
Program
ya COD kwa Shule za Sekondari Bumbuli itahusisha makubaliano kati ya
Shirika la Maendeleo Bumbuli, Shule za Sekondari Bumbuli na Halmashauri
ya Wilaya kulipa jumla ya kiasi cha Dola za kimarekeni 100 kwa kila
mwanafunzi anayefaulu mitihani ya kidato cha IV kwa daraja la I-III.
Malipo ya COD yatafanyika baada ya uthibitisho wa matokeo ya mtihani wa
kidato cha nne. Fedha zitapelekwa Halmashauri ya Wilaya, Shule za
Sekondari na kwa walimu na wanafunzi. Fedha zitakazogawiwa kwa shule
zitatumika kwa ajili ya mahitaji ya kielimu ya shule kama zilivyowekewa
vipaumbele na Bodi za Shule.
Watakaonufaika na mradi:
Kwa
kila mwanafunzi atakayefaulu mtihani (Div I-III) anapomaliza kidato
cha nne, Shirika la Maendeleo Bumbuli kupitia program ya COD litatoa
malipo yafuatayo:
1. Walimu: Tsh 60,040/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
2. Wanafunzi: Tsh 50,500/= Kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
3. Shule: Tsh 31,600/= Kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
4. Halmashauri ya Wilaya: Tsh 15,800/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
Vipimo na Ukaguzi:
Data
za mitihani kuanzia mwaka 2011 zitatoa msingi wa awali, na msingi huo
utakuwa ukibadilishwa kila mwaka na ufanisi wa utendaji wa shule, hivyo
kila mwaka unakuwa msingi kwa ajili ya malipo ya mwaka ujao wa.
Kiashiria cha matokeo kitakuwa idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu kidato
cha nne kwa kupata daraja la I-III. Ili kuyadumisha matokeo hayo,
hatua mbalimbali zitakuwa vikiripotiwa kila mwaka na shule na
halmashauri. Mkataba, matokeo, na taarifa nyingine zitawekwa wazi kwa
wananchi ili kuongeza uwajibikaji wa wafadhili na wapokeaji
Shirika
la Maendeleo Bumbuli halina nia ya kusema kwamba COD ndio suluhisho
pekee la tatizo la maendeleo ya elimu au ufumbuzi wa matatizo yote
katika mfumo wa elimu nchini lakini tunaamini inaonesha matarajio ya
kutosha kuona thamani ya kujaribu, kujifunza na kutathmini.
Uendelevu wa program
Ili
program iwe endelevu, Shirika la Maendeleo Bumbuli(BDC) litaweka mfumo
thabiti wa kufanya tathimini na kutoa mrejesho, ambao utatumika kama
zana ya kupimia uwajibikaji, na kuendeleza uwazi. Pia ni muhimu
kuzingatia ushirikishwaji wa wenyeji wa Bumbuli na umiliki wa program ya
COD. Hili linaweza kufanikiwa kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha
elimu bora kama uwekezaji wa wenyeji, na Mtandao wa Wahitimu wa Shule za
Sekondari Bumbuli kwa ajili ya fedha za COD. Zaidi sana, Shirika la
Maendeleo Bumbuli litahusisha na kutumia Bodi za Shule, ambazo
zinahusisha wazazi na walimu. Hii ndiyo njia itakayowafanya watu wa
Bumbuli wathamini juhudi zao wenyewe katika kuboresha jamii zao.
5. Kambi ya Wanafunzi Wanaojiandaa na Mtihani wa Kidato cha Nne 2012
Kuanzia
tarehe 4 Agosti hadi 5 Septemba, wakati wa likizo za masomo, Shirika
limeandaa kambi maalum kwa matayarisho ya vijana wanaojiandaa na mtihani
wa Kidato cha Nne mwaka huu. Kambi hii itakuwepo kwenye Kituo cha
Elimu Soni, ambacho kina mandhari, mazingira na eneo la kutosha
kufundishia na kuishi wanafunzi katika kipindi hiki.
Kila
siku, wanafunzi hao watapigwa msasa kwa masomo ambayo hawakupata fursa
ya kuyasoma vizuri katika mwaka wa shule, watafundishwa mbinu za
kufanya mitihani (ikiwemo time-management), na kufanya revision ya
mitihani ya Kidato cha Nne ya kuanzia mwaka 1984 hadi sasa. Shirika
litatafuta walimu wenye sifa za kufundisha masomo ya Hesabu,
Kiingereza, Historia, Kemia, Fizikia na Biolojia, hata nje ya Jimboni
na kuwalipa posho kuja kufundisha kwenye kambi. Pia tutaomba watu
mbalimbali, ikiwemo walimu wastaafu, wenye moyo wa kujitolea waje
kufundisha kambi hii.
Mwisho
Hadi
sasa Shirika la Maendeleo Bumbuli halijapata mfadhili au ufadhili
kutoka kokote au kwa mtu yoyote. Miradi hii niliyoitaja ndio iko katika
hatua za kupata ufadhili. Fedha ambazo zimetumika hadi sasa kuanzisha
Shirika, kuweka ofisi, kuajiri watumishi wa muda na kufanya utafiti na
kutengeneza maandiko ya miradi zimetokana na mkopo niliouchukua kama
Mbunge, ikiwemo mkopo wa gari ambao sikuutumia kununua gari bali
kuanzisha Shirika.
Napenda
kutoa mwito kwa wana-Bumbuli wenzangu na Watanzania kwa ujumla
kusaidia kuchangia maendeleo ya Jimbo la Bumbuli, hasa kwa miradi
ambayo hatukuitafutia ufadhili kama huu wa COD na kambi. Kwa
kuchangia unaweza kutumia namba ya M-PESA 0762088050. Kwa maelezo zaidi
kuhusu Shirika la Maendeleo Bumbuli, tuma barua pepe: getinvolved@bumbuli.org au piga simu: +255 22 2129821/6 au tuma fax: +255 22 2129796
Katika miezi ijayo, BDC pia itatekeleza
miradi ya kitaifa yenye manufaa kwa maendeleo na utawala bora kwa nchi
yetu. Naamini nchi yetu itapiga hatua za maendeleo kwa kasi zaidi kama
kila mmoja wetu, kwa nafasi na uwezo wake, atathubutu, lakini pia kama
sote tutasaidiana katika kuchangiana na kupeana mawazo kuhusu shughuli
za maendeleo.
No comments:
Post a Comment