Thursday, July 12, 2012


 
Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa  kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi  kama kilele kimojawapo  cha maisha yangu ya utumishi  wa umma.  Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu.  Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.

No comments:

Post a Comment